Pesa za elimu ya bure zafujwa Kenya
Uchunguzi uliofanywa na tume ya kupambana na
ufisadi nchini Kenya umefichua kuwa walimu
wakuu nchini humo walifuja pesa za elimu ya
bure kwa shule za msingi katika taifa hilo.
Walimu wakuu wanadaiwa kutumia pesa
zilizotengwa kununua vifaa vya shule kama vile
vitabu kwa masuala tofauti.
Wakuu hao wanalaumiwa kwa kutumia pesa za
vitabu kugharamia safari za nje na kujilipa
marupurupu.
Hali hii inalaumiwa kusababisha uhaba wa vitabu
na dawati katika maelfu ya shule za msingi
nchini Kenya. Aidha baadhi ya walimu wakuu
waliwakopesha wazazi pesa hizo bila ya wazazi
kuzirudisha.
Kulingana na ripoti hiyo, shule nyinginezo
zilipokea pesa hizo kupitia akaunti ya shule
tofauti. Hili limetiliwa shaka kwani kila shule
inastahili kupokea pesa kwa akaunti yake kwa
minajili ya uwajibikaji.
Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiangi alilaumu
kutokuwepo kwa namna ya kuzuia ufujaji. '
Kwa upande wake, afisa mkuu mtendaji wa tume
ya maadili na kupambana na ufisadi nchini
Kenya, Halakhe Wako, amesema kuwa serikali ya
Kenya inastahili kuwachukulia hatua walimu
husika ili kukomesha tabia hiyo.
Mapema mwaka huu rais Uhuru Kenyatta
alimuagiza waziri Matiangi kuanzisha uchunguzi
juu ya jinsi fedha za elimu ya bure
zinavyotumika.
Mnamo mwaka wa 2010 mataifa ya marekani na
Uingereza yalisimamisha ufadhili wao kwa wizara
ya elimu na kusema kuwa hatua hio ilitokana na
wizi wa fedha za elimu ya buire.
Serikali ya Kenya hutumia shilingi bilioni 14 kila
mwaka kufadhili elimu ya bure.
No comments