TAARIFA KAMILI KUHUSU AJALI YA BASI LA HBS LILILOKUWA LINATOKA MBEYA KUELEKEA TABORA NA KUUA WATU WA NNE NA KUJERUHI 29.MBEYA
Mwonekano wa Basi la Hbs Express mara Baada ya kupata Ajali katika Eneo la Maji Mazuri katika Barabara ya kutoka Mbeya kwenda Chunya.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
Wasamalia wema wakiokoa watu waliokuwa wamenasa ndani ya Basi hilo(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
Polisi wa Usalama Barabarani akitoa maelezo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makalla mara Baada ya kufika katika eneo la Ajali (Picha na David Nyembe wa Fahari News)
wananchi wakiwa wamembeba Mmoja wa walionusurika katika Ajali Hiyo(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
Baadhi ya vijana wakiwa wanachimba shimo ili kuweza kutoa mwili wa mmoja wa Abilia aliyekuwa ameminywa na Basi hilo.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
mtoto wa miaka 15 Yakob Mahonga ambaye ni mmoja wa abiria aliyenusurika katika ajali hiyo, aliweza kuwaokoa baadhi ya abiria kwa kuwafungua mikanda, kisha kuvunja vioo vya basi ili waweze kujiokoa akimwelezea Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makalla Mara Baada ya kufika katika Hospitali ya Rufaa jinsi alivyokuwa akiwasaidia abiria.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Amosi Makalla akimpa pole mama na Mwanae walionusurika katika Ajali Hiyo katika Hospitali ya Rufaa(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
WATU wanne wamepoteza maisha na 29 kujeruhiwa katika ajali ya basi la abiria aina ya scania lenye namba za usajili T273 AHV mali ya kampuni ya HBS baada ya kuacha njia na kupinduka kandokando ya barabara katika eneo la Maji mazuri lililopo Wilayani Mbeya.
Basi hilo likiendeshwa na dereva Nassoro Hemedy, linalofanya safari zake za mikoani lilikuwa likitokea Mkoani Mbeya na kuelekea Mkoani Tabora, lilipata ajali hiyo majira ya saa mbili za asubuhi, baada ya kudaiwa kufeli breki na kisha kupinduka.
Katika ajali hiyo, watu wanne ambao wanawake wawili na wanaume wawili walipoteza maisha huku 29 wakijeruhiwa lakini kwa mujibu wa taarifa ya muuguzi wa zamu wa hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Jesca Kahangwa majeruhi 20 hali zao si nzuri na wanaendelea kupatiwa matibabu.
Aidha, katika hali isiyokuwa ya kawaida, mtoto wa miaka 15 Yakob Mahonga ambaye ni mmoja wa abiria aliyenusurika katika ajali hiyo, aliweza kuwaokoa baadhi ya abairia kwa kuwafungua mikanda, kisha kuvunja vioo vya basi ili waweze kujiokoa.
Akizungumza mtoto huyo ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Arusha, amesema kuwa alikuwa akisafiri na mjomba wake kuelekea Wilayani Chunya kwa ajili ya kwenda kumuona mgonjwa.
“Tulipofika katika eneo la Kawetele mbali kidogo na eneo la ajali mimi nikiwa nimekaa pembeni ya dereva nilianza kuhisi kwamba gari hilo linatatizo baada ya kumuona dereva akiwa anahangaika,”alisema.
Alisema, walipofika kituo kingine cha mbele gari hiyo ilisimama na kasha kondakta wa gari na dereva walishuka na kuanza kurekebisha baadhi ya vitu vilivyokuwa haviko sawa chini ya gari, lakini walihangaika kutafuta maji na kuyakosa na safari kuendelea.
“Dereva na kondakta walinijibu kuwa hawafahamu zilipo na kubaki ni kimshuhudia dereva akiruka kutokea dirishani, lakini nilihangaika kutafuta spana hizo na kufanikiwa kuzipata na kuanza kuwafungua abiria mikanda na kisha kuvunja vioo vya basi ili waweze kutoka nje,”alisema.
Akizungumzia ajali hiyo kwenye eneo la tukio, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amosi Makala, ambaye mbali na kutoa pole kwa majeruhi lakini alitumia nafasi hiyo kuliagiza jeshi la polisi Mkoani Mbeya, kitengo cha usalama barabarani kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa magari katika kituo cha mabasi kabla ya kuanza safari zake.
Hata hivyo, Mkuu huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Mbeya,alikitaka kitengo cha uslama wa barabarani kutoa taarifa ni kwanini gari hilo liliruhusiwa kusafiri huku likiwa limebeba abiria zaidi ya 80.
“Nimeambiwa gari hili lilikuwa limebeba abiria waliokuwa wamesimama si chini ya 20 kutoka stendi ya mabasi, hivyo ninawataka wahusika kunipa maelezo ya kutosha na kwa hili, sintalifumbia macho wahusika wa uzembe huu watawajibika hatuwezi kuweka maisha ya watu rehani,”alisema.
Mwisho.
No comments