Silaa Adai Wafuasi wa Chadema walitishia Kuchoma Nyumba yake

ALIYEKUWA mgombea ubunge wa Ukonga,
Jerry Silaa (CCM) amedai kuwa wafuasi wa
Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) walimtishia kuchoma moto
nyumba yake wakati wa Uchaguzi Mkuu
uliofanyika mwaka jana.
Silaa alieleza hayo jana katika Mahakama
Kuu Kanda ya Dar es Salaam, wakati akitoa
ushahidi wa kesi ya kupinga matokeo
yaliyompa ushindi mbunge wa jimbo hilo,
Mwita Waitara (Chadema).
Alitoa ushahidi huo kwa njia ya kiapo baada
ya Jaji Fatuma Msengi kutupilia mbali
pingamizi la upande wa walalamikiwa
waliokuwa wanapinga kupokewa kwa kiapo
hicho kwa kuwa kina mapungufu kisheria.
Katika kiapo hicho, Silaa anaeleza kuwa,
Oktoba 27 mwaka jana katika kituo cha
kujumlishia kura cha Pugu Sekondari,
kulikuwa na idadi kubwa ya wapiga kura wa
Chadema wakiwa wamesimama mita 20
kutokea usawa wa kituo hicho.
Alidai kuwa wafuasi hao walianza kuwatishia
Mawakala na Msimamizi wa Kituo, jambo
lililosababisha Polisi washindwe kufanya kitu
zaidi ya kuwaonya, ndipo mjibu maombi wa
pili na wenzake wakasema hawatopokea
matokeo na watachoma moto nyumba yake
pamoja na kituo hicho.
Silaa ambaye aliwahi kuwa, Meya wa
Manispaa ya Ilala, alidai hadi Oktoba 27,
baadhi ya vituo vilikuwa havijakusanya
matokeo jambo lililosababisha aandike barua
kwenda kwa Msimamizi wa Kituo kuomba
mchakato wa kuhesabu kura urudiwe.

No comments