Madaktari wa Tanzania wafanya upasuaji wa moyo bila kutumia mashine ya kusimamisha moyo na mapafu

Tanzania inaendelea kupiga hatua katika nyanja
ya afya baada ya madaktari wa Tanzania katika
hospitali ya taifa ya Muhimbili, Taasisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete, wakishirikiana na wenzao wa
India wamefanikiwa kufanya upasuaji wa moyo
wa aina yake Tanzania.
Upasuaji huo ujulikanao kama ‘bypass surgery’
ulishirikisha kupandikizwa kwa mishipa ya damu
kutoka sehemu nyingine ya mwili moyoni bila
kutumia mashine ya kusimamisha moyo na
mapafu.
Kwa kawaida madaktari wanasema upasuaji wa
moyo hufanyika baada ya moyo na mapafu
kusimama, lakini upasuaji huo ulifanyika wakati
moyo na mapafu vikifanya kazi.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa
Bashir Nyangasa ameambia BBC kuwa upasuaji
huo wa kupandikiza mishipa ya damu nje ya
mshine ni wa kihistoria nchini Tanzania.
“Mgonjwa anaweza kutolewa mishipa ya damu
kutoka miguuni au mikononi baada ya kupewa
dawa ya usingizi na mishipa hiyo kupandikizwa
kwenye mshipa wa moyo uliokuwa umeziba ili
kuruhusu mzunguko wa damu wa moyo kama
kawaida bila kutumia mashine,” amesema.
Upasuaji huo wa moyo kwa njia ya kupandikiza
umefanyika kwa watu wawili, ambao umeonesha
mafanikio makubwa kwa kuwa hali zao
zinaendelea vizuri .
Dkt Nyangasa amesema kwa sasa hakuna haja
ya Watanzania wenye matatizo ya moyo kwenda
nje ya nchi kwa kuwa wao kama wataalam
wameweza kufanya upasuaji huo.
Anasema madaktari sasa wanaweza kuhudumia
wagonjwa wengi zaidi wenye uhitaji na
kupunguza gharama kwa serikali ya kusafirisha
wagonjwa wa moyo nje ya nchi.
Mwandishi wa BBC aliyepo Dar es Salaam
Esther Namuhisa anasema wengi wa wagonjwa
wamekuwa wakisafiri hadi India ambapo wengi
hukumbana na changamoto nyingi kupata
huduma hiyo kifedha na hata kwenye upande wa
lugha.

No comments