Rais Magufuli Awasili Nchini Uganda Leo Kuhudhuria Sherehe Za Kuapishwa Rais Museveni
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 11 Mei, 2016 amewasili Jijini Kampala nchini Uganda ambapo kesho anatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Mteule wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni.
Rais Magufuli ametua katika uwanja wa ndege wa Entebe majira ya saa tano za asubuhi na kupokelewa na Waziri wa Ujenzi na usafirishaji wa Uganda Mheshimiwa John Byabagambi na kisha kuelekea Ikulu ya Entebe ambako amepokelewa rasmi na mwenyeji wake Mheshimiwa Rais Yoweri Kaguta Museveni.
Akiwa katika Ikulu ya Entebe Rais Magufuli amekagua gwaride rasmi lililoandaliwa kwa heshima yake na pia amepigiwa mizinga 21.
Aidha, Viongozi hao wamefanya mazungumzo ambapo pamoja na kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano na uhusiano kati ya nchi hizo mbili, Rais Magufuli amemhakikishia Rais Museveni kuwa Tanzania itatoa ushirikiano wa kutosha kufanikisha ujenzi wa bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka Hoima katika Ziwa Albert nchini Uganda na kupita kaskazini mwa Tanzania hadi bandari ya Tanga.
Rais Magufuli ameongozana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Mheshimiwa Suzan Kolimba.
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Kampala
11 Mei, 2016
No comments